CRDB yaunga mkono upanuzi wa huduma za uwekezaji nchini


Na Charles Mkoka

Benki ya CRDB Plc imesema ushirikiano kati ya taasisi za fedha ni muhimu katika kukuza ubunifu wa kifedha na kuimarisha soko la mitaji nchini.

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa uzinduzi wa hatifungani ya kampuni ya iTrust Finance Limited yenye thamani ya Tshs bilioni 100 uliofanyika Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Masoko ya Kimataifa wa CRDB, Barton Mwasamengo alisema taasisi hiyo imehusika kama mshauri mkuu wa muamala, wakala wa mauzo, msajili, mlezi wa dhamana pamoja na benki ya kupokea malipo katika hatifungani hiyo ya kwanza ya iTrust.

Barton amesema kuwa uzinduzi huo ni hatua muhimu kwa ukuaji wa soko la mitaji Tanzania na utaongeza nafasi za kampuni kupata fedha za muda mrefu kwa ajili ya biashara na uwekezaji.

“Ubunifu wa kifedha hauwezi kufanyika kwa taasisi moja pekee. Unahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali za kifedha na wawekezaji,” alisema Barton Mwasamengo.

Hatifungani za kampuni zinaendelea kuwa njia muhimu ya kusaidia biashara kupata mtaji huku zikiongeza fursa za uwekezaji kwa taasisi na wananchi wa kawaida.

Benki hiyo imefanya kazi kwa karibu na iTrust pamoja na wataalamu wa sheria na wahasibu kuhakikisha hatifungani hiyo inaendana na matarajio ya wawekezaji pamoja na malengo ya kampuni.

CRDB pia ilieleza kuwa mfumo wake wa benki utatumika kupokea maombi ya uwekezaji kwenye hatifungani hiyo, hatua inayolenga kurahisisha wananchi na taasisi kushiriki.

Uzinduzi huo unakuja wakati Tanzania ikiendelea kushuhudia ongezeko la matumizi ya soko la mitaji kama chanzo mbadala cha upatikanaji wa fedha kwa kampuni binafsi na taasisi za kifedha.

Hatifungani ya iTrust inatarajiwa kuorodheshwa katika Dar es Salaam Stock Exchange baada ya kufungwa kwa mauzo yake mwezi Juni mwaka huu.