Watu wanne wauawa Kenya katika maandamano ya bei ya mafuta

Na Mwandishi wetu, Nairobi

Nairobi. Watu wasiopungua wanne wamefariki dunia na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa nchini Kenya baada ya maandamano makubwa ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta na gharama za maisha kuzuka katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, watu 348 wamekamatwa kufuatia vurugu, uharibifu wa mali pamoja na mapambano kati ya waandamanaji na polisi.

Maandamano hayo yalizua taharuki kubwa katikati ya mji baada ya madereva wa usafiri wa umma (matatuu) kugoma kazi huku baadhi ya barabara zikifungwa kwa matairi yaliyokuwa yakichomwa moto.

Wananchi wengi walilazimika kutembea kwa miguu kwenda kazini baada ya huduma za mabasi na matatu kusimama katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo.

Hasira za wananchi zimeongezeka baada ya kupanda kwa bei ya mafuta kunakosababisha gharama kubwa za usafiri, chakula na bidhaa nyingine muhimu huku wananchi wengi wakilalamikia ugumu wa maisha.

Serikali ya Rais imesema ongezeko hilo limechangiwa na bei za mafuta duniani pamoja na changamoto za usambazaji zinazohusishwa na mvutano wa Mashariki ya Kati.

Akizungumza jijini Nairobi, Murkomen alisema serikali inaheshimu haki ya wananchi kuandamana lakini haitaruhusu vurugu wala uporaji.

“Tunaiheshimu haki ya maandamano ya amani, lakini vitendo vya uhalifu na uharibifu wa mali havitavumiliwa,” alisema.

Baada ya presha kuongezeka, serikali ilitangaza kupunguza bei ya dizeli kwa Shilingi 10 za Kenya kwa lita na kuanza mazungumzo na viongozi wa sekta ya usafiri ili kutuliza hali.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa maandamano wameonya kuwa mgomo unaweza kurejea ikiwa serikali haitatoa suluhisho la kudumu kuhusu gharama za maisha.

Maandamano hayo pia yameongeza presha kwa serikali ya Ruto ambayo imekuwa ikikosolewa kwa sera za uchumi na kupanda kwa gharama za maisha tangu ilipoingia madarakani.

Wachambuzi wa uchumi wanasema hali hiyo inaonyesha namna kupanda kwa bei ya mafuta duniani kunavyoendelea kuathiri mataifa mengi ya Afrika yanayotegemea mafuta kutoka nje.