Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi wa kampuni ya JD Core Stores, Joanita Cornellius Mutayoba, amesema wafanyabiashara wengi wa Tanzania wamekuwa wakikumbana na changamoto kubwa za kupata vibali vya kuuza bidhaa katika soko la China kutokana na ucheleweshaji wa mfumo wa GACC, hali ambayo imekuwa ikiwafanya baadhi yao kuachana na biashara hizo.
Mutayoba alitoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa “Zero Tariff for Shared Opportunities” uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, uliowakutanisha wafanyabiashara, serikali na wadau wa biashara kujadili namna ya kunufaika na fursa mpya za soko la China.
Mkutano huo uliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na serikali ya China kufuatia utekelezaji wa sera mpya ya zero tariff kwa bidhaa kutoka nchi za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na Beijing.
Kwa mujibu wa Mutayoba, mchakato wa kupata vibali kupitia mfumo wa GACC unaweza kuchukua hadi miaka miwili au mitatu, jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa wafanyabiashara wengi.
“Sisi Tanzania tunakuwa upande wa kupoteza kwa sababu China wao wanapata bidhaa kutoka nchi nyingine wakati sisi tunachelewa,” alisema.
Alisema kuna haja ya serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, TanTrade au ubalozi wa Tanzania nchini China kuwapeleka wataalamu kujifunza kwa kina namna ya kuendesha mfumo huo ili kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania.
Mutayoba alisema maboresho ya mfumo huo yatafungua fursa za ajira, kukuza uchumi na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa, hususan kwa wanawake wanaojihusisha na biashara za mazao, vyakula na bidhaa za uchumi wa buluu.
“Wanawake wengi kwenye biashara hizi wamekuwa wakipitia changamoto kwa ukimya mkubwa,” alisema.
Aliongeza kuwa yuko tayari kwenda kujifunza zaidi kuhusu mfumo huo ili kusaidia wafanyabiashara wengine nchini kufahamu taratibu za kuuza bidhaa katika soko la China.
Kauli yake inaakisi changamoto ambazo zimekuwa zikielezwa na wafanyabiashara wengi wa Tanzania kuhusu urasimu wa mifumo ya export, licha ya kuongezeka kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China.