Na Mwandishi wetu
DAR ES SALAAM — China imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania wakati nchi hizo mbili zikiadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia, huku Beijing ikitangaza rasmi utekelezaji wa sera ya zero tariff kwa bidhaa kutoka Afrika.
Akizungumza katika mkutano wa kifungua kinywa wa “Zero Tariff for Shared Opportunities” kwa exporters wa Tanzania uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema sera hiyo imeanza kutekelezwa rasmi kuanzia Mei 1, 2026.
Kwa mujibu wa balozi huyo, bidhaa zote kutoka nchi za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China sasa zitaingia katika soko la China bila ushuru chini ya mfumo wa sasa wa tariff line.
“Hii ni sera kubwa yenye manufaa kwa nchi za Afrika,” alisema Chen. “Bidhaa zote kutoka Afrika zilizopo kwenye mfumo wa tariff line sasa hazitalipiwa ushuru zinapoingia China.”
Alisema hatua hiyo itasaidia bidhaa za Tanzania kupata njia ya haraka na yenye ufanisi kuingia katika soko kubwa la watumiaji wa China, hususan mazao ya kilimo, madini na bidhaa za utamaduni.
Kwa mujibu wa Chen, sera hiyo pia inatarajiwa kuongeza faida na ushindani kwa wazalishaji wa Tanzania huku ikichochea maendeleo ya viwanda, ajira na ustawi wa wananchi.
Kauli hiyo imekuja wakati China na Tanzania zikiadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia ambao umeendelea kuwa miongoni mwa ushirikiano wa muda mrefu na wa kimkakati kati ya China na Afrika.
Katika kipindi hicho, ushirikiano wa nchi hizo mbili umejikita katika sekta za miundombinu, biashara, usafirishaji, viwanda, nishati na utamaduni, huku China ikiendelea kuwa mmoja wa washirika wakubwa wa maendeleo na biashara wa Tanzania.
Balozi Chen aliwahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kujifunza kwa haraka vigezo na taratibu za kuuza bidhaa katika soko la China ili waweze kutumia kikamilifu fursa hiyo mpya.
“Ninafahamu mwanzo huwa mgumu, lakini safari ya maili elfu moja huanza kwa hatua moja,” alisema.
Aliongeza kuwa ubalozi wa China nchini Tanzania uko tayari kushirikiana na wafanyabiashara wa Tanzania ili kuwasaidia kuelewa vizuri sera hiyo na kuitumia kwa manufaa ya pamoja.
Mkutano huo uliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na serikali ya China, ukihusisha viongozi wa serikali, wawekezaji, exporters na wadau wa sekta binafsi.