Serikali kuunda mkakati mpya wa kuwezesha wafanyabiashara kunufaika na soko la nje


Na Charles Mkoka

Serikali imepanga kuanzisha dawati maalum la kusaidia mauzo ya bidhaa kwenda China chini ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), ikiwa ni sehemu ya mageuzi mapya ya kurahisisha biashara na kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika zaidi na soko la nje ya nchi, ikiwemo China.

Hatua hiyo ilitangazwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, wakati wa mkutano wa kifungua kinywa wa “Zero Tariff for Shared Opportunities” uliowakutanisha exporters wa Tanzania katika hoteli ya Johari Rotana.

Mkutano huo uliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na serikali ya China, ukihusisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, wafanyabiashara na wadau wa biashara kujadili namna ya kuongeza mauzo ya Tanzania kwenda China.

Kwa mujibu wa Kapinga, dawati hilo litakuwa na maafisa biashara wanaozungumza lugha ya Kichina pamoja na maafisa watakaoratibu moja kwa moja na ubalozi na mamlaka husika ili kusaidia wafanyabiashara kushughulikia changamoto za lugha, taratibu za biashara na uratibu wa soko hilo.

“China ni mshirika wetu mkubwa wa kibiashara, hivyo tunahitaji mikakati ya kipekee kuhakikisha wafanyabiashara wetu wanalifikia soko hilo kwa ufanisi,” alisema.

Kapinga alisema serikali sasa inabadilisha mfumo wake wa utendaji kazi kutoka udhibiti kwenda uwezeshaji wa wafanyabiashara, akisisitiza kuwa taasisi za umma zinapaswa kusaidia wafanyabiashara kufikia viwango vinavyotakiwa badala ya kuwazuia.

“Si sahihi tena mfanyabiashara kuambiwa hana vigezo bila kusaidiwa namna ya kuvifikia,” alisema.

Alikiri kuwa wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikumbana na changamoto za uratibu kati ya taasisi mbalimbali pamoja na mfumo wa GACC wa China, hasa kutokana na changamoto za lugha na mawasiliano.

Kwa mujibu wa waziri Kapinga, serikali itaimarisha uratibu kati ya taasisi zote zinazohusika na biashara ya nje ili kuhakikisha mfanyabiashara anapata msaada kuanzia hatua ya mwanzo hadi kufanikisha mauzo yake nje ya nchi.

Aidha, serikali imepanga kuimarisha mifumo ya kidijitali katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupunguza urasimu na kuongeza uwazi katika ufuatiliaji wa maombi ya wafanyabiashara.

Kapinga alipongeza taasisi kama TBS na BRELA kwa hatua zilizopigwa katika mifumo ya kidijitali huku akiitaka TanTrade kuongeza kasi ya maboresho.

Serikali pia imepanga kuanzisha Jukwaa la Wafanyabiashara wa Mauzo ya Nje (Exporters Forum), litakalokuwa likifanyika kwa njia ya ana kwa ana na mtandao kwa kila sekta ya bidhaa zinazouzwa nje.

Mpango huo utaendeshwa kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Kilimo, kutokana na sekta ya kilimo kuwa miongoni mwa zinazoongoza katika mauzo ya Tanzania kwenda China.

Kapinga pia aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza katika kuongeza thamani ya bidhaa, usindikaji, ubunifu na matumizi ya chapa ili kuongeza ushindani katika soko la China na kimataifa.

Alisema fursa ya biashara na China inapaswa kutazamwa zaidi ya suala la kuondolewa kwa kodi, bali kama jukwaa la kuongeza ajira, kukuza viwanda na kuongeza kipato kwa wakulima na wazalishaji nchini.