Marekani Yafanya Operesheni Ya Kijeshi Caracas Kwa Ndege Maalum Za Osprey

 

Jeshi la Marekani limetekeleza zoezi maalum la kijeshi katika ubalozi wake uliopo Caracas nchini Venezuela, likihusisha ndege za kijeshi aina ya MV-22B Osprey zinazoweza kuruka kama helikopta na pia kusafiri kwa kasi kama ndege za kawaida. 

Zoezi hilo lilifanyika Mei 23, 2026 na kuonekana kuwa moja ya operesheni kubwa za kijeshi za Marekani nchini humo tangu kurejea kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mapema mwaka huu. 

Kwa mujibu wa Ubalozi wa Marekani mjini Caracas, operesheni hiyo ilikuwa ni mazoezi ya “rapid response” kwa ajili ya kujiandaa na dharura za kitabibu au majanga yanayoweza kuhitaji uokoaji wa haraka wa wafanyakazi wa kidiplomasia. 

Mashuhuda waliona ndege mbili za MV-22B Osprey zikizunguka anga la Caracas kabla ya kutua ndani ya eneo la ubalozi huku wanajeshi wa Marekani wakishuka kwa haraka kufanya mazoezi ya operesheni maalum. 

Kamanda wa Marekani anayesimamia operesheni za kijeshi katika Amerika Kusini kupitia United States Southern Command, Jenerali Francis Donovan, alihudhuria zoezi hilo akiwa ndani ya moja ya ndege hizo na kufanya mazungumzo na viongozi wa mpito wa Venezuela. 

Serikali ya Venezuela ilisema ilikuwa imeidhinisha zoezi hilo mapema kama sehemu ya maandalizi ya dharura za kiafya au majanga makubwa. 

Tukio hilo limezua mjadala mkubwa nchini Venezuela huku baadhi ya wananchi wakieleza wasiwasi kuhusu uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani nchini humo.

Kumekuwa na waandamanaji wachache mitaani, wakionekana na na jumbe mbalimbali za kupinga operesheni hiyo. 

Zoezi hilo limekuja miezi michache baada ya Marekani kufungua tena ubalozi wake Caracas kufuatia mabadiliko makubwa ya kisiasa yaliyotokea nchini Venezuela mapema mwaka huu.

Soma na hapa

pia soma