Mkuu Wa BTI: TFS Yavunja Mitazamo, Wanawake Wazidi Kung'ara Sekta Ya Ufugaji.

Katika miaka ya nyuma, sekta ya ufugaji nyuki ilionekana kuwa kazi ngumu inayowafaa zaidi wanaume kutokana na mazingira yake ya kazi ikiwemo kutundika mizinga juu ya miti na kufanya shughuli katika maeneo ya misitu. Hata hivyo, taswira hiyo sasa imeanza kubadilika kwa kasi huku wanawake wengi wakijitokeza kujiunga na mafunzo ya ufugaji nyuki nchini.

Mabadiliko hayo yanaonekana wazi katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki (BTI) kilichopo mkoani Tabora, ambapo idadi ya wanafunzi wanawake imeongezeka kwa kiwango kikubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Akizungumza na vyombo vya habari Mei 21, 2026, Mkuu wa Chuo hicho, Semu Daud amesema kwa sasa wanawake wanachukua nafasi kubwa zaidi katika sekta hiyo tofauti na ilivyokuwa zamani.

“Ukilinganisha na miaka ya nyuma wanawake wengi sasa wamejikita katika shughuli za ufugaji nyuki. Kwa sasa chuo kina wanafunzi takribani 350 ambapo asilimia 54 ni wanaume na asilimia 46 ni wanawake, na lengo letu ni kufikia uwiano wa 50 kwa 50 na inawezekana kabisa,” amesema Semu.

Ameeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na mwamko mkubwa wa jamii, matumizi ya teknolojia za kisasa za ufugaji nyuki pamoja na jitihada za Serikali na wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya nyuki nchini.

Kwa mujibu wa Semu, teknolojia mpya zimebadili kabisa mazingira ya kazi yaliyokuwa yakionekana kuwa magumu kwa wanawake.

“Zamani kozi za maliasili zilikuwa na wavulana wengi kutokana na mazingira ya kazi yenyewe, hasa kutundika mizinga katika miti. Lakini sasa mizinga inatundikwa katika vichanja na matumizi ya teknolojia bora na salama yamerahisisha kazi hata kwa wanawake,” amesema.

Katika mafanikio hayo, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetajwa kuwa nguzo muhimu katika mageuzi ya sekta ya ufugaji nyuki nchini kupitia uwekezaji mkubwa unaofanywa katika mafunzo, miundombinu na mafunzo kwa vitendo.

Semu amesema TFS imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika chuo hicho hatua ambayo imeongeza ubora wa mafunzo na kuwavutia vijana wengi zaidi kujiunga na sekta hiyo.

Mbali na hilo, wanafunzi wengi wa BTI hupata nafasi ya kwenda katika vituo mbalimbali vya TFS nchini kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, jambo linalowasaidia kuoanisha maarifa ya darasani na hali halisi ya kazi.

“TFS ni mdau mkubwa sana kwa sababu ndio wamiliki wakubwa wa misitu nchini. Karibu wanafunzi wetu wote wanapelekwa katika vituo vya TFS kupata mafunzo kwa vitendo ili wakajifunze zaidi na kuoanisha kile walichojifunza darasani,” amesema.

Ukuaji wa ushiriki wa wanawake katika ufugaji nyuki unaonekana kuwa ishara ya mabadiliko mapana ndani ya sekta ya maliasili nchini, huku TFS ikiendelea kujenga mazingira rafiki ya ushiriki wa makundi yote katika uchumi wa kijani, uhifadhi wa misitu na maendeleo endelevu.

Kupitia uwekezaji huo, TFS si tu inalinda rasilimali za misitu na nyuki, bali pia inaendelea kufungua fursa mpya za ajira, ujasiriamali na usawa wa kijinsia kwa vijana wa Kitanzania.

Soma