Serikali ya Botswana imekanusha taarifa iliyosambaa mitandaoni ikidai kuwa Rais Duma Boko ametangaza siku maalum ya mapumziko kwa mashabiki wa Arsenal kusherehekea ubingwa wa Ligi kuu ya Uingereza (EPL).Barua hiyo ya uzushi ilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii Jumatano asubuhi ikiwa na nembo na muhuri unaofanana na wa Serikali ya Botswana, hali iliyowafanya baadhi ya watu kuamini kuwa ilikuwa taarifa rasmi.
Katika barua hiyo, Rais Boko alidaiwa kuwapa mashabiki wa Arsenal ruhusa ya kutokwenda kazini ili kusherehekea ushindi wa klabu hiyo.
Taarifa hiyo ilisababisha baadhi ya mashabiki kufurahia kwa utani na wengine kutaka kujua kama ni kweli serikali ilikuwa imetoa tamko hilo, au laa.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Ofisi ya Rais wa Botswana ilitoa taarifa rasmi ikisema barua hiyo ni ya uongo na haijatolewa na serikali.
Serikali pia imewaonya wananchi kuhusu kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa, huku ikiwataka kutumia vyanzo rasmi vya serikali kupata taarifa sahihi.