Serikali kupitia Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) imeendelea kuongeza ukaguzi wa vipimo kwenye biashara mbalimbali nchini huku wafanyabiashara wakionywa dhidi ya matumizi ya mizani na vipimo batili.
Ukaguzi huo unalenga kulinda watumiaji, kuhakikisha ushindani wa haki pamoja na kusaidia serikali kupata takwimu sahihi za uchumi.
Kwa sasa, maeneo yanayopewa kipaumbele kwenye ukaguzi ni pamoja na masoko, maduka, vituo vya mafuta, maghala, bidhaa zilizofungashwa pamoja na mitungi ya gesi ya kupikia.
Katika vituo vya mafuta, WMA inaendelea kuhakiki pampu za mafuta kuhakikisha kiwango kinacholipiwa na mteja ndicho kinachotolewa.
Kwa upande wa masoko na maduka, ukaguzi mkubwa umeelekezwa kwenye matumizi ya mizani za kielektroniki na vipimo vya bidhaa kama sukari, mchele, nyama na nafaka.
WMA pia imezindua kampeni mpya Kariakoo na maeneo mengine ya jijini Dar es Salaam kupinga matumizi ya makopo, mafungu na vipimo visivyo rasmi kwenye biashara.
Serikali imekuwa ikiongeza nguvu na juhudi katika kudhibiti udanganyifu wa vipimo unaoweza kuwaumiza walaji na kuathiri biashara zilizo halali.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Ufugaji imeishauri serikali kuanza kuhakiki hata vipimo vya vifurushi vya simu na intaneti (maarufu kama bando) kufuatia malalamiko ya watumiaji kuhusu madai ya bando kuisha haraka isivyo kawaida.
Kwa mujibu wa sheria, kila mfanyabiashara anayetumia kifaa cha kupimia, anatakiwa kuhakiki kifaa hicho kila mwaka kupitia WMA na kupata muhuri rasmi wa usalama.
Wafanyabiashara watakaobainika kutumia vipimo batili wanaweza kutozwa faini ya hadi Tsh milioni 20, kifungo cha miaka miwili jela au vyote kwa pamoja.
