Na Charles Mkoka
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia kikamilifu katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki nchini huku ikiimarisha uwezo wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika utekelezaji wa sheria za mazingira.Akizungumza kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amesema serikali inaendelea na mkakati mpana wa kukabiliana na changamoto za mazingira ikiwemo uchafuzi wa mazingira unaotokana na plastiki na usimamizi wa taka ngumu.
Masauni amesema pamoja na mipango ya muda mrefu ya kuimarisha taasisi za mazingira, hatua za kisheria dhidi ya wanaoendelea kukiuka marufuku ya mifuko ya plastiki zinaendelea kuchukuliwa kupitia sheria zilizopo na usimamizi wa NEMC.“Serikali haipo likizo. Tunaendelea kuchukua hatua dhidi ya wote wanaoendelea kukiuka sheria hizi,” amesema Masauni huku akitoa wito kwa wananchi kuacha matumizi ya mifuko ya plastiki kwa ajili ya kulinda mazingira.Amesema serikali inaendelea kuimarisha NEMC ili iweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira na kutoa suluhisho endelevu kwa changamoto za kimazingira nchini.
Aidha, amesema serikali kwa kushirikiana na TAMISEMI pamoja na Wizara ya Ujenzi inaendelea kushughulikia changamoto za taka ngumu na miundombinu katika maeneo mbalimbali ikiwemo jijini Dar es Salaam.Masauni pia ametambua mchango wa wakusanyaji taka binafsi, wanaharakati wa mazingira na wananchi wanaojitolea katika shughuli za uhifadhi wa mazingira, akisema juhudi zao ni sehemu muhimu ya mkakati wa taifa wa kulinda mazingira.NEMC, ambayo inatimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, imeendelea kuwa taasisi muhimu katika usimamizi wa mazingira nchini kupitia utoaji wa elimu, usimamizi wa tathmini za athari za mazingira pamoja na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya mazingira. Serikali imeeleza dhamira ya kuendelea kuimarisha mamlaka na uwezo wa taasisi hiyo kadri Tanzania inavyoelekea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050