Akizungumza wakati wa kutangaza maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, alisema kaulimbiu ya mwaka huu ya taifa, “Dira ya 2050: Tuwajibike kuikijanisha Tanzania”, inalenga kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.
Masauni alisema maadhimisho ya mwaka huu yanaenda sambamba na ajenda ya kimataifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa vitendo, huku Tanzania ikiendelea kuimarisha juhudi zake katika uhifadhi wa misitu, matumizi ya nishati safi za kupikia na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira.
Kwa mujibu wa serikali, matumizi ya nishati safi za kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.69 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, hatua inayotajwa kusaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.Aidha, serikali imeonya kuhusu ongezeko la taka ngumu nchini, zikikadiriwa kufikia kati ya tani milioni 30 hadi 60 kwa mwaka ifikapo 2050 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Tuna wajibu wa pamoja kuhakikisha maendeleo tunayoyapata hayaathiri mazingira na maisha ya vizazi vijavyo,” alisema Masauni.
Maadhimisho hayo yatahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo upandaji miti, usafi wa mazingira, kongamano la vijana kuhusu mazingira, maonyesho ya teknolojia na ubunifu wa mazingira pamoja na mikutano ya kisayansi.Kongamano la kisayansi na utafiti wa mazingira, ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC pamoja na Kongamano la Wadau wa Mazingira, litafanyika Mei 28, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam na linatarajiwa kushirikisha washiriki takriban 1,000 kutoka Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki.
Aidha, maonyesho ya teknolojia na ubunifu kuhusu uhifadhi wa mazingira yatafanyika Dodoma kuanzia Juni 1 hadi Juni 5, 2026 yakihusisha wizara, taasisi za umma, sekta binafsi, vijana na asasi za kiraia, huku yakitarajiwa kuwa na mabanda takriban 100.Serikali pia imetangaza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika Dodoma Juni 5, 2026, ambapo pia itazinduliwa Programu ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu ya Tanzania 2026–2030.

