Kituo cha kaboni chapewa Tshs bilioni 5 kuimarisha mifumo

 

Serikali imeongeza kasi ya kuimarisha biashara ya kaboni nchini huku ikitenga Tshs bilioni 5 kwa ajili ya kuimarisha Kituo cha Kaboni cha Taifa, hatua inayolenga kufanya biashara hiyo kuwa moja ya vyanzo vikuu vya mapato kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, alisema kituo hicho sasa kitapata hadhi ya kujitegemea na tayari kimepewa ofisi za kudumu eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Awali kituo hicho kilikuwa chini ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, lakini sasa kina bodi yake ya wakurugenzi, watumishi wa kutosha pamoja na mifumo mipya ya uendeshaji kwa ajili ya kuimarisha biashara ya kaboni nchini.


Tumejipanga kuhakikisha biashara ya kaboni inakuwa moja ya vyanzo vikubwa vya fedha katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050,” alisema Dkt. Muyungi.

Alisema serikali itaendelea kuongeza uwekezaji wa muda mfupi, wa kati na wa muda mrefu ili kukifanya kituo hicho kuwa kitovu muhimu cha biashara ya kaboni kwa Tanzania na Afrika.

Katika hatua nyingine, Dkt. Muyungi alisema Tanzania imefanikiwa kushinda ushindani dhidi ya Nairobi, Addis Ababa na Dakar kupewa ofisi mpya ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa hasara na uharibifu.



Dkt. Muyungi pia aliipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, akisema taasisi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika elimu ya mazingira, usimamizi wa miradi, utekelezaji wa sheria pamoja na kuiwezesha Tanzania kupata ushirikiano na fedha za kimataifa za mazingira.

Serikali pia imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki huku ikihimiza ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Soma