Na Mwandishi wetu
Wataalamu wa afya duniani wamewataka wananchi kupima shinikizo la damu mara kwa mara huku wakionya kuwa ugonjwa huo unaendelea kuua watu wengi kimya kimya.
Wito huo umetolewa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Damu Duniani yanayoadhimishwa Mei 17 kila mwaka.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu takribani bilioni 1.4 duniani wanaishi na shinikizo la damu, lakini wengi wao hawajui kama wana tatizo hilo.
WHO imeeleza kuwa ugonjwa huo hujulikana kama “silent killer” kwa sababu mara nyingi hauna dalili za wazi lakini unaweza kusababisha kiharusi, magonjwa ya moyo, figo pamoja na vifo vya mapema.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema, “Controlling Hypertension Together: Check Your Blood Pressure Regularly, Defeat the Silent Killer.”
Barani Afrika, wataalamu wa afya wanasema shinikizo la damu linaongezeka kutokana na mabadiliko ya maisha, vyakula vyenye chumvi nyingi, matumizi ya pombe, uvutaji sigara pamoja na ukosefu wa mazoezi.
Kwa mujibu wa WHO, Afrika ndiyo eneo lenye kiwango kikubwa zaidi cha watu wenye shinikizo la damu duniani, ambapo takribani asilimia 27 ya watu wazima wanaishi na tatizo hilo.
Nchini Tanzania, tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa takribani watu watatu kati ya 10 wana shinikizo la damu, huku wengi wao wakikosa vipimo vya mara kwa mara.
Wataalamu wa afya nchini wanasema changamoto kubwa ni watu wengi kugundua tatizo hilo baada ya kupata madhara makubwa kama kiharusi au matatizo ya moyo.
“Watu wengi hawapimi presha mpaka wanapopata shida kubwa kiafya. Kupima mapema kunaweza kuokoa maisha,” amesema mhudumu mmoja wa afya jijini Dar es Salaam.
WHO imeshauri wananchi kula vyakula vyenye chumvi kidogo, kufanya mazoezi, kuacha sigara, kupunguza matumizi ya pombe pamoja na kufuata ushauri wa madaktari kuhusu dawa.
Wataalamu wa afya wanaendelea kusisitiza kuwa kupima shinikizo la damu ni hatua rahisi lakini muhimu katika kuzuia madhara makubwa ya kiafya.
