Katika taarifa iliyotolewa Mei 15, 2026, Ofisi hiyo imesema ukurasa huo unaotumia jina la “Give Direct Foundation” umekuwa ukiwahamasisha wananchi kuomba fedha kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi wamekuwa wakitakiwa kuchagua kiwango cha fedha wanachotaka kisha kulipa ada ya usajili ili kupata fedha hizo.
Ofisi ya Makamu wa Rais imesema wahusika wa utapeli huo wanatumia picha ya Dkt. Nchimbi ili kuwafanya wananchi waamini kuwa ukurasa huo ni rasmi.
Hata hivyo, Serikali imesisitiza kuwa haina uhusiano wowote na ukurasa huo wala matangazo yake.
“Taarifa hizo si za kweli na Makamu wa Rais hahusiki kwa namna yoyote na shughuli hizo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Wananchi wametakiwa kuwa makini na kuepuka kufanya malipo yoyote yanayohusiana na matangazo ya aina hiyo.
Pia wamehimizwa kuripoti ukurasa huo kupitia mfumo wa Facebook kwa kutumia kipengele cha “Report Ad”.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais imewataka wananchi waliopata hasara au wenye taarifa kuhusu tukio hilo kuwasiliana na Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Katika miaka ya karibuni, matukio ya utapeli mtandaoni yameongezeka nchini huku baadhi ya wahalifu wakitumia majina ya viongozi wa serikali, taasisi na watu maarufu kuwashawishi wananchi kutuma fedha.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Charlii Media wamesema elimu zaidi kuhusu usalama wa matumizi ya mitandao inahitajika ili kupunguza matukio ya utapeli wa kidijitali.
