Na Mwandishi wetu
DODOMA — Makamu wa Rais wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, ametembelea banda la Rural Energy Agency (REA) katika kilele cha Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yanayoendelea jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, Nchimbi alipatiwa maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na nishati jadidifu inayotekelezwa na wakala huo nchini.
Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala wa REA, Advera Mwijage, alisema miradi hiyo imechangia kupunguza matumizi ya nishati zinazoharibu mazingira na kusaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya vijijini.
Alieleza kuwa upatikanaji wa nishati safi na ya uhakika unaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za Tanzania katika kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maonesho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu ya "Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania", ikisisitiza umuhimu wa ushiriki wa kila mmoja katika kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu.
