Daraja jipya kuwakomboa wananchi Mtwara vijijini


Na Mwandishi wetu, 

Mtwara. Wakulima wa korosho na ufuta katika Kata za Kitele na Mnima sasa wana sababu ya kutabasamu baada ya kukamilika kwa daraja jipya la mita 21 lililojengwa katika barabara ya Chekereni–Mkonye–Nambela.

Daraja hilo limejengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia Mradi wa RISE unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Kwa miaka mingi, eneo hilo lilikuwa likikumbwa na changamoto za mafuriko yaliyokatiza mawasiliano, hasa wakati wa mvua kubwa.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Mtwara, Khatibu Nunu, amesema daraja hilo limeondoa kikwazo kikubwa kilichokuwa kikiathiri usafirishaji wa mazao kwenda sokoni.

“Korosho na ufuta ni mazao makuu ya biashara hapa. Zamani malori yalikuwa yanapata shida kuvuka eneo hili hasa wakati wa msimu wa mavuno,” amesema.

Mbali na biashara, daraja hilo pia limeboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wanaotegemea Kituo cha Afya Kitele na zahanati za jirani.

Mkazi wa Chekereni, Jema Mchewa, amesema daraja la zamani lilikuwa jebamba na mara nyingi kufunikwa na maji wakati wa mafuriko.

“Mvua zikiongezeka, watu walikuwa wanahofia kuvuka. Sasa hali imebadilika kabisa,” amesema.

Naye Saidi Mpunga amesema wagonjwa walilazimika kubebwa kwa mikono kuvuka mto wakati wa mafuriko ili kufikishwa hospitali.

“Leo hii magari yanapita bila shida. Hii ni faraja kubwa kwa wananchi,” amesema.

Wananchi wanasema daraja hilo limeongeza usalama kwa wanafunzi, wajawazito na wakulima ambao sasa wanaweza kusafiri na kusafirisha mazao yao mwaka mzima bila hofu ya kukwama njiani.