Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kuwa kitovu cha sekta ya kilimo barani Afrika mwezi Septemba mwaka huu wakati likiandaa toleo la 10 la Africa Agri Expo 2026, tukio kubwa linalowakutanisha wakulima, wawekezaji, viongozi wa biashara, watunga sera na wabunifu wa teknolojia za kilimo kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Maonesho hayo yatakayofanyika Septemba 2 hadi 3, 2026 katika viwanja vya Sabasaba, ukumbi wa Mwandoro Hall huku ikienda sambamba na Future Food Livestock & Poultry Expo, yakilenga kuunganisha wadau wa mnyororo mzima wa chakula kuanzia uzalishaji wa mazao, mifugo, usindikaji, teknolojia na biashara.
Waandaaji wa maonesho hayo wamesema toleo la mwaka huu linafika katika kipindi ambacho Afrika imeendelea kuvutia wawekezaji wengi kutokana na kuwa na zaidi ya asilimia 60 ya ardhi ya kilimo ambayo bado haijatumika duniani pamoja na ongezeko kubwa la mahitaji ya chakula.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAB Group, Tahir Abdul Bari, amesema Afrika si soko la kesho bali ni soko la sasa, na kampuni zitakazojenga mahusiano ndani ya bara hilo sasa zitakuwa sehemu ya viongozi wa biashara ya chakula katika miaka ijayo.
"Afrika si soko la baadaye, ni soko la leo. Biashara zitakazowekeza na kujenga mahusiano hapa sasa ndizo zitakazoongoza kizazi kijacho cha biashara ya kilimo na chakula duniani," amesema.
Kwa Tanzania, maonesho hayo yanaweka Dar es Salaam katika nafasi muhimu kama lango la biashara kwa Afrika Mashariki na Kati kutokana na nafasi yake ya kimkakati, miundombinu ya bandari inayokua na jitihada za kuimarisha sekta ya kilimo.
Washiriki watapata fursa ya kujionea teknolojia mpya za kilimo, mifumo ya umwagiliaji, mashine za kisasa, pembejeo, kilimo kidijitali pamoja na suluhisho za kuongeza thamani baada ya mavuno.
Kupitia eneo maalum la sekta ya mifugo na chakula, wadau pia watajadili masuala ya lishe ya mifugo, huduma za mifugo, teknolojia za uzalishaji, mifumo ya kuhifadhi chakula katika mnyororo wa baridi pamoja na vifaa vya usindikaji.
Aidha, kutakuwa na mijadala ya kitaalamu itakayowakutanisha wataalamu wa kilimo, viongozi wa Serikali, wawekezaji na wabunifu kujadili masuala muhimu yanayoligusa bara la Afrika ikiwemo kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula, upatikanaji wa fedha za kilimo na nafasi ya vijana katika kuleta mapinduzi ya kilimo.
Waandaaji wamesema maonesho hayo yatatoa fursa kwa kampuni kuonesha bidhaa na huduma zao, kupata washirika wapya wa biashara, kufungua masoko mapya pamoja na kujenga mahusiano ya muda mrefu katika moja ya sekta zinazokua kwa kasi duniani.
Baada ya mafanikio ya matoleo tisa yaliyopita, Africa Agri Expo 2026 inatarajiwa kuwa toleo kubwa zaidi kuwahi kufanyika kwa kuleta pamoja biashara, ubunifu na uwekezaji utakaosaidia kuandika sura mpya ya kilimo cha Afrika.
