Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema mafanikio ya uhifadhi wa mazingira nchini yanahitaji ushiriki wa pamoja wa wananchi, taasisi za umma, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha rasilimali za asili zinaendelea kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Kupitia ushiriki wake katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, NEMC imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu wajibu wao katika kulinda mazingira na kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali za taifa.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Kanda ya Kati wa NEMC, Bw. Novatus Mushi, amesema masuala ya mazingira yanagusa kila sekta ya maendeleo, hivyo kila mwananchi ana nafasi ya kuchangia katika uhifadhi wake.
"Mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu. Mafanikio katika uhifadhi wake yanategemea uwajibikaji na ushirikiano wa pamoja kati ya wananchi na wadau wote wa maendeleo," amesema Mushi.
Amesema kupitia banda la NEMC, wananchi wanapata elimu kuhusu usimamizi wa taka, upandaji na utunzaji wa miti, matumizi sahihi ya rasilimali za mazingira pamoja na kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia shughuli za maendeleo.
Aidha, NEMC pia inaonesha mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo maboresho ya huduma za mazingira kupitia mifumo ya kidijitali inayorahisisha wananchi na wadau kupata huduma mbalimbali kwa haraka zaidi.
Kwa mujibu wa NEMC, ushiriki katika Wiki ya Utumishi wa Umma umeendelea kuwa fursa muhimu ya kuwafikia wananchi moja kwa moja, kuongeza uelewa kuhusu masuala ya mazingira na kuhimiza utamaduni wa kuhifadhi rasilimali za asili kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.

