TANESCO yaondoa hofu ya matumizi ya umeme kwenye vyombo vya usafiri

Na Mwandishi wetu, Dodoma.

TANESCO yaondoa hofu ya matumizi ya umeme kwenye vyombo vya usafiri

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema wananchi hawapaswi kuwa na hofu ya kutumia vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme, huku likieleza kuwa linaendelea kujenga vituo vya kuchajia magari, pikipiki na vyombo vingine vya usafiri wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, alipotembelea banda la shirika hilo katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Twange amesema Tanzania inaelekea kwenye matumizi makubwa ya nishati safi, si tu kwenye kupikia bali pia katika sekta ya usafiri, na kwamba TANESCO imeanza kuonesha mfano kwa kutumia baadhi ya vyombo vyake vya usafiri vinavyotumia umeme.

"Tumejipanga kujenga vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme nchi nzima. Wananchi wasiogope kutumia teknolojia hii kwa sababu sisi kama wazalishaji wa umeme tunaendelea kuhakikisha huduma inapatikana kwa uhakika," amesema Twange.

Katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Twange amesema TANESCO kwa kushirikiana na sekta binafsi ina mpango wa kusambaza takribani majiko sanifu ya umeme milioni moja ndani ya miaka miwili hadi mitatu kupitia mfumo unaowezesha wananchi kulipa gharama zake kidogo kidogo kupitia ununuzi wa Luku.

Amesema mpango huo ni sehemu ya jitihada za kuondoa hofu kwa wananchi kuhusu matumizi ya umeme kupikia na kuongeza matumizi ya nishati safi inayolinda mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TANESCO, Bi. Beatrice Kimoleta, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kutembelea banda hilo na kujionea namna watumishi wanavyotoa huduma kwa wananchi.

Amesema TANESCO inaendelea kujivunia watumishi wake wanaotoa huduma kwa ubunifu, weledi na kujituma kwa lengo la kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na za uhakika.

"Tunawaomba wateja wetu waendelee kutuamini. Tunafahamu umeme ni huduma muhimu kwa maisha na maendeleo ya kila Mtanzania, hivyo tunaendelea kuongeza jitihada za kuboresha huduma na kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na nishati ya umeme," amesema Kimoleta.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanaendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23, yakiwa na kaulimbiu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”

Soma