Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tume ya Ushindani (FCC) imesema inaendelea kuongeza juhudi za kuwaelimisha wananchi kuhusu haki za mlaji, ushindani wa haki wa biashara na madhara ya bidhaa bandia, huku ikitangaza mpango wa kuanzisha Vilabu vya Ushindani katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu.
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa FCC, Bi. Roberta Feruzi, amesema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kusogeza huduma za Tume karibu na wananchi.
Amesema wananchi wanaotembelea banda la FCC wanapata elimu kuhusu haki zao kama walaji, namna ya kutambua bidhaa bandia, masuala ya ushindani wa biashara pamoja na fursa ya kuwasilisha malalamiko na kupata ufumbuzi wa papo kwa papo.
"Wiki ya Utumishi wa Umma inatupa nafasi ya kukutana ana kwa ana na wananchi, kuwaeleza majukumu yetu na kushughulikia changamoto wanazozifikisha kwetu," amesema Feruzi.
Kwa mujibu wa Feruzi, mpango wa kuanzisha Vilabu vya Ushindani unalenga kujenga kizazi chenye uelewa kuhusu umuhimu wa ushindani wa haki, kufanya maamuzi sahihi wakati wa kununua bidhaa na huduma, pamoja na kutambua haki na wajibu wao kama walaji.
Amesema elimu hiyo ya mapema itasaidia kujenga jamii yenye uelewa mkubwa wa masuala ya biashara na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya taifa, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kukuza uchumi.
Feruzi amewahimiza wananchi kuendelea kutembelea banda la FCC katika maonesho hayo au kutumia namba maalum ya bure ya Tume ili kupata taarifa, kuwasilisha malalamiko na kupata huduma zinazohusu ushindani, ulinzi wa mlaji na bidhaa bandia.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma huwakutanisha taasisi mbalimbali za Serikali na wananchi kwa lengo la kuonesha huduma zinazotolewa, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa jamii.
