Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) limewataka wajasiriamali nchini kuacha kutegemea kuuza mazao na malighafi katika hali yake ya kawaida na badala yake kuwekeza katika uchakataji, ubora wa bidhaa na vifungashio ili kuongeza thamani na kipato.
Afisa Masoko wa SIDO, Bi. Antonia Masoi, amesema Tanzania ina rasilimali nyingi za kilimo, mifugo na uvuvi ambazo zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha viwanda vidogo na ajira endapo zitachakatwa na kuongezewa thamani.
"Tunataka kuona wananchi wanabadilika kutoka kuuza mazao ghafi kwenda kuzalisha bidhaa zenye thamani zaidi. Mahindi yanaweza kuwa unga, karanga zinaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali. Huko ndiko kunakoongeza kipato na kujenga biashara imara," amesema Masoi.
Amesema SIDO inaendelea kuwasaidia wajasiriamali kupitia mafunzo ya kitaalamu, matumizi ya teknolojia sahihi, ushauri wa biashara, kuboresha ubora wa bidhaa pamoja na kuwatafutia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Masoi, SIDO ina vituo vya teknolojia katika mikoa saba nchini vinavyolenga kuendeleza teknolojia zinazotumia malighafi zinazopatikana Tanzania ili kuongeza thamani ya bidhaa za wazalishaji wa ndani.
Ameongeza kuwa pamoja na uzalishaji, wajasiriamali wanafundishwa masuala ya ubora, utambulisho wa bidhaa, uwekaji wa lebo na vifungashio ili kuwawezesha kushindana katika masoko makubwa.
SIDO pia huwapatia wajasiriamali fursa ya kutangaza bidhaa zao kupitia maonesho mbalimbali ya biashara, huku maonesho ya kitaifa ya mwaka huu yakitarajiwa kufanyika Kahama kuanzia Oktoba 21 hadi 30.
Katika kusaidia ukuaji wa biashara, SIDO pia inaunganisha wajasiriamali na fursa mbalimbali za fedha ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Ujasiriamali na Ubunifu (NEDIF), mifumo ya dhamana ya mikopo pamoja na programu za ufadhili kupitia washirika wa maendeleo na ushirikiano na CRDB Foundation kwa ajili ya vijana.
Masoi amewataka hasa vijana kutumia fursa hizo kuanzisha viwanda vidogo vitakavyoongeza ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Pia amewaonya wazalishaji wa bidhaa kama sabuni, vipodozi na bidhaa nyingine zinazotengenezwa majumbani kutegemea taarifa zisizo sahihi kutoka mitandaoni bila kupata mafunzo rasmi.
"Usikimbilie kuangalia video mtandaoni na kuanza kutengeneza bidhaa bila maarifa sahihi. Njoo SIDO upate mafunzo, teknolojia na mwongozo ili uzalishe bidhaa zenye ubora zinazoweza kukubalika sokoni," amesema
Ameongeza kuwa SIDO itaendelea kushirikiana na wajasiriamali katika safari ya kujenga viwanda vidogo imara na kukuza uchumi wa Tanzania.
"Njoo SIDO, tushirikiane kuzungusha gurudumu la uchumi na kujenga Tanzania ya viwanda," amesema Masoi.
