RFB YAELEZA JINSI TOZO ZA MAFUTA ZINAVYOCHANGIA BARABARA BORA NCHINI

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wananchi waliotembelea banda la Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma wamepata elimu kuhusu namna tozo za mafuta zinavyosaidia kugharamia matengenezo ya maelfu ya kilomita za barabara nchini.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa RFB, Mhandisi Rashid Kalimbaga, amesema tozo zinazotozwa kwenye mafuta ya petroli na dizeli ndizo chanzo kikuu cha fedha zinazowezesha matengenezo ya barabara za Tanzania.

Amesema mfumo huo umewekwa ili kuhakikisha mtandao wa barabara unabaki salama, unapitika kipindi chote cha mwaka na kuendelea kusaidia shughuli za uchumi na maisha ya wananchi.

"Fedha zinazotokana na tozo za mafuta zina mchango mkubwa katika kuhakikisha barabara zetu zinapata matengenezo ya mara kwa mara na zinaendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi," amesema Mhandisi Kalimbaga.

Mbali na tozo za mafuta, amesema Mfuko wa Barabara pia hupata mapato kupitia tozo zinazolipwa na magari ya kigeni yanayotumia mtandao wa barabara nchini, ambapo fedha hizo huelekezwa katika matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS pamoja na TARURA.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kalimbaga, kwa sasa RFB inafadhili matengenezo ya zaidi ya kilomita 181,000 za barabara nchini, mtandao ambao unaunganisha maeneo ya uzalishaji, masoko, shule, vituo vya afya na huduma nyingine muhimu za kijamii.

Ameeleza kuwa uwekezaji katika matengenezo ya barabara unaendelea kuwa nguzo muhimu ya kukuza uchumi kwa kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kufungua fursa za maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mhandisi Kalimbaga amewahimiza wananchi kuendelea kutembelea banda la RFB ili kupata taarifa zaidi kuhusu majukumu ya Mfuko wa Barabara, vyanzo vyake vya mapato na namna fedha hizo zinavyorejesha thamani kwa Watanzania kupitia miundombinu bora.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanaendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma yakiongozwa na kaulimbiu isemayo, “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”