WANANCHI WATAKA ELIMU YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI IANZE MASHULENI

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Wananchi wameitaka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kuongeza wigo wa utoaji elimu kuhusu faragha na ulinzi wa taarifa binafsi kwa kuanzia katika ngazi za shule ili kujenga kizazi kinachotambua haki na wajibu wa kulinda taarifa zake.

Ushauri huo umetolewa na mkazi wa Dodoma, Bw. Fred Nyandoro, baada ya kutembelea banda la PDPC katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma na kupata elimu kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi.

Bw. Nyandoro amesema kutoa elimu hiyo kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo kutasaidia kujenga jamii inayoheshimu faragha pamoja na matumizi sahihi ya taarifa za watu.

"Tukiwaelimisha vijana mapema kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi, tutakuwa tunajenga jamii inayojitambua na inayoheshimu faragha za wengine. Pia kila mmoja anapaswa kuwa makini na namna anavyotunza taarifa zake," amesema.

Kupitia maonesho hayo yanayoendelea kuanzia Juni 16 hadi 23, 2026, PDPC inaendelea kutoa elimu na ushauri kwa wananchi na watumishi wa umma kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, pamoja na wajibu wa kulinda taarifa binafsi katika matumizi ya kila siku.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yameendelea kuwa jukwaa la kuzikutanisha taasisi za Serikali na wananchi kwa lengo la kutoa huduma, kupokea maoni na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu majukumu mbalimbali ya taasisi hizo.