Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Zaidi ya wananchi 300 kutoka maeneo mbalimbali nchini wametembelea banda la Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali, Dodoma, kupata elimu na ufafanuzi kuhusu miradi ya barabara katika maeneo yao.
Ushiriki huo umeendelea kuimarisha mawasiliano kati ya TARURA na wananchi, ambapo wageni wanaotembelea banda hilo wanapata nafasi ya kuwasilisha kero, kuuliza maswali na kupewa majibu ya moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa wakala huo.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa TARURA, Bi. Catherine Sungura, amesema wananchi wengi wanaofika katika banda hilo hutaka kufahamu maendeleo ya ujenzi na matengenezo ya barabara katika maeneo yao, huku baadhi yao wakiunganishwa moja kwa moja na Mameneja wa TARURA wa mikoa na wilaya husika kwa maelezo zaidi.
“Tunapokea wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania. Wengi wanakuja na maswali kuhusu barabara zao, hivyo tunawahusisha wataalamu wa maeneo husika ili wapate majibu sahihi na ya haraka,” amesema Bi. Sungura.
Amesema lengo la TARURA ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miradi inayotekelezwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuboresha mtandao wa barabara za wilaya.
Miongoni mwa wananchi waliopata huduma ni Bi. Sarah James Joseph, mkazi wa King’ongo, Kimara jijini Dar es Salaam, aliyefika katika banda hilo kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa barabara ya TRA–King’ongo.
Kupitia mawasiliano na Meneja wa TARURA Wilaya ya Ubungo, alipatiwa ufafanuzi kuwa barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha zege imefikia hatua nzuri, ambapo kilomita 1.6 zimebaki kukamilika. Kati ya hizo, mita 800 zinatarajiwa kuanza kujengwa kuanzia Julai mwaka huu, huku sehemu iliyosalia ikitekelezwa katika hatua inayofuata.
Akizungumza baada ya kupata maelezo hayo, Bi. Sarah ameishukuru TARURA kwa kutoa fursa kwa wananchi kufika moja kwa moja na kupata taarifa kuhusu miradi inayowagusa.
Kwa upande wake, Bi. Sungura amesema TARURA itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri, biashara na upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yalianza Juni 16 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23 yakibeba kaulimbiu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”


