Daraja la Mambi lafungua njia ya uchumi, kupunguza gharama za usafiri Mtwara

 

Na Mwandishi Wetu, Mtwara

Wakazi wa kata za Mtimbwilimbwi, Njengwa na Hinju katika Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara wameanza kunufaika na matunda ya ujenzi wa Daraja la Mambi, mradi uliomaliza changamoto ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa masika na kurahisisha usafirishaji wa mazao pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 13 lililojengwa katika barabara ya Chiwindi–Mtimbwilimbwi kupitia Mradi wa RISE chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), ni sehemu ya programu ya kuondoa vikwazo katika miundombinu ya barabara (Road Bottleneck Programme).

Meneja wa TARURA Wilaya ya Mtwara, Mhandisi Khatibu Nunu, amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo, wananchi wa maeneo ya Majengo, Mtimbwilimbwi, Njengwa na Hinju walikuwa wakikwama kuvuka Mto Mambi wakati wa mvua kutokana na maji kujaa.

Amesema hali hiyo ilikuwa ikichelewesha usafirishaji wa mazao muhimu ya biashara kama korosho na ufuta kutoka mashambani kwenda maghala ya Vyama vya Msingi, huku pia ikiwazuia wananchi kufikia huduma za afya, elimu na huduma za kiutawala zilizopo upande wa Mji wa Nanyamba.

"Daraja hili limekuwa kiunganishi muhimu kwa wananchi wa maeneo haya kufika barabara kuu ya Mtwara–Nanyamba–Tandahimba na kupata huduma mbalimbali kwa urahisi zaidi," amesema Mhandisi Nunu.

Kwa wananchi, mradi huo umeondoa adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwalazimu kurudi nyumbani bila kufika mashambani au kutumia njia ndefu zenye gharama kubwa.

Bi. Amina Ally Ayandike, mkazi wa kata ya Mtimbwilimbwi, amesema hapo awali maji ya Mto Mambi yalikuwa kikwazo kikubwa hasa wakati wa msimu wa mvua.

"Tulikuwa tunaenda mashambani lakini tunarudi njiani kwa sababu mto umejaa maji. Sasa hivi hakuna anayeshindwa kwenda shambani kwa sababu ya maji. Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia huduma hii," amesema.

Naye mkazi mwingine, Bw. Juma Mohamed Henda, amesema daraja hilo limepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafiri.

Amesema awali gharama ya bodaboda kutoka Mtimbwilimbwi hadi Nanyamba ilikuwa Sh15,000, huku magari yakitoza kati ya Sh40,000 hadi Sh45,000 kutokana na kulazimika kupita njia za mzunguko, lakini baada ya kukamilika kwa daraja hilo gharama zimepungua hadi takribani Sh5,000.

Ujenzi wa Daraja la Mambi ni miongoni mwa miradi ya miundombinu inayotekelezwa kupitia Mradi wa RISE unaolenga kuboresha barabara za vijijini, kuimarisha usafiri na usafirishaji pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.