Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umesema mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja umeendelea kuimarisha upatikanaji wa mafuta nchini kwa kutumia mfumo wa zabuni za ushindani unaozingatia mabadiliko ya bei katika soko la dunia.
Kupitia mfumo huo, PBPA hupanga zabuni za kuwapata wasambazaji wa mafuta, kusimamia mikataba na kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa wakati licha ya mabadiliko ya bei na changamoto zinazoweza kujitokeza katika soko la kimataifa.
PBPA imeeleza kuwa mikataba ya ununuzi wa mafuta hutumia utaratibu wa M+2, ambapo mchakato wa kupanga na kuingia mikataba hufanyika mapema ili kuhakikisha mafuta yanayoagizwa yanawasilishwa kwa wakati na kuepusha changamoto za upungufu wa mafuta nchini.
Katika mchakato wa zabuni, kampuni mbalimbali hushindana kwa kutoa bei nafuu za mafuta pamoja na gharama za usafirishaji, hatua inayosaidia kupata huduma kwa ufanisi zaidi huku ikizingatia hali halisi ya soko la kimataifa.
Aidha, PBPA imebainisha kuwa sekta ya mafuta huathiriwa kwa kiasi kikubwa na matukio ya kimataifa ikiwemo migogoro ya kivita na changamoto za usafiri wa majini, ambazo zinaweza kuchelewesha usafirishaji au kuongeza gharama za mafuta.
Kutokana na hali hiyo, mfumo wa M+2 umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kupanga mahitaji ya nchi mapema na kuhakikisha usambazaji wa mafuta haukatiki hata wakati wa changamoto katika soko la dunia.
Kwa sasa, mfumo wa usambazaji nchini unazingatia pia uwepo wa akiba ya mafuta kwenye maghala inayoweza kukidhi matumizi ya takribani siku 23, hatua inayoongeza uhakika wa upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa shughuli za uchumi na maisha ya kila siku.
PBPA imeendelea kusisitiza usimamizi madhubuti wa zabuni na mikataba ya mafuta ili kuhakikisha wananchi na sekta mbalimbali za uzalishaji zinaendelea kupata mafuta kwa uhakika wakati wote.
