TFS yawakaribisha wananchi kujifunza fursa za misitu katika Wiki ya Utumishi wa Umma

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeendelea kutumia Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa misitu, utalii wa misitu na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika sekta hiyo.

Maonesho hayo yanayofanyika kuanzia Juni 16 hadi 23, 2026 yamekuwa jukwaa kwa TFS kuonesha huduma zake mbalimbali, ikiwemo usimamizi endelevu wa misitu, uzalishaji wa mazao ya misitu, fursa za uwekezaji pamoja na bidhaa zinazotokana na rasilimali za nyuki.

Miongoni mwa vivutio katika banda la TFS ni elimu kuhusu udungishaji wa nyuki (Apitherapy), tiba asilia inayotumia sumu ya nyuki kwa madhumuni mbalimbali ya kiafya, ambapo wananchi wanapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wataalamu na kujifunza kuhusu huduma hiyo pamoja na bidhaa nyingine zinazotokana na nyuki.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mhifadhi Mkuu wa TFS, Kassim Ally, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kutembelea banda la wakala huo ili kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali kupitia TFS.

"Tuna fursa nyingi katika sekta ya misitu kuanzia utalii, uwekezaji, bidhaa za nyuki hadi mazao mbalimbali ya misitu. Wananchi wafike banda letu wapate elimu na kujionea kazi zinazofanyika katika kuhifadhi na kuendeleza rasilimali hizi muhimu," amesema.

TFS inaendelea kutekeleza jukumu la kuhifadhi na kusimamia rasilimali za misitu nchini kwa kuzingatia matumizi endelevu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda mazingira, kuchochea uchumi wa kijani na kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo.