Mhe. Ridhiwani Kikwete avutiwa na mfumo wa kidijitali wa REA kusimamia miradi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kutumia teknolojia ya kidijitali katika kupanga, kufuatilia na kusimamia miradi ya nishati vijijini.

Ridhiwani ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea banda la REA wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo, Waziri huyo alivutiwa na mfumo wa REA Digital Platform, mfumo wa kisasa unaowezesha ufuatiliaji wa miradi yote inayotekelezwa na REA na kutoa taarifa kwa wadau mbalimbali popote walipo duniani.

Akitoa maelezo kuhusu mfumo huo, Afisa Upimaji Mwandamizi wa REA, Bw. Hussein Shamdas, amesema mfumo huo unamwezesha mwananchi kuona mipango ya miradi ya REA katika eneo lake na kufuatilia hatua za utekelezaji wake kwa uwazi zaidi.

Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yanaimarisha uwazi, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi pamoja na wadau wa sekta ya nishati.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yamezikutanisha taasisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kuonesha maboresho yanayofanyika katika utoaji wa huduma za umma.