PBPA yasogeza elimu ya mafuta karibu na wananchi Dodoma

 Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) imeshiriki Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mfumo wa uagizaji wa mafuta na mchango wake katika sekta ya nishati nchini.

Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi Juni 17, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Wiki ya Utumishi wa Umma ni jukwaa muhimu linalowakutanisha wananchi na taasisi za Serikali ili kuwapa huduma, elimu na taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Mafuta wa PBPA, Bw. Issa Mwitazy, amesema ofisi yake inatumia maonesho hayo kueleza namna Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja unavyosaidia kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini, kuimarisha uwazi katika biashara ya mafuta na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta hiyo.

Amesema wananchi wanaotembelea banda la PBPA wanapata nafasi ya kujifunza kuhusu majukumu ya PBPA pamoja na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo.

“Tunatumia maonesho haya kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu namna mfumo wa uagizaji mafuta unavyofanya kazi na mchango wake katika kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta wakati wote,” amesema.

PBPA imesema ushiriki wake katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mawasiliano na wadau mbalimbali huku ikiendelea kutoa elimu kuhusu mchango wa mfumo huo katika kuimarisha usalama wa nishati na kukuza uchumi wa Taifa.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”