Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imeitaka TANESCO kuongeza idadi ya vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuendelea kuharakisha matumizi ya nishati safi nchini.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, alipotembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Ridhiwani ameipongeza TANESCO kwa hatua zinazochukuliwa katika kuhamasisha matumizi ya umeme kwenye sekta ya usafiri pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“TANESCO mnafanya kazi kubwa. Nawapongeza kwa mageuzi ya matumizi ya nishati ya umeme katika vyombo vya usafiri. Natoa rai muongeze vituo vya kuchajia vyombo hivyo ili kuongeza wigo wa utoaji huduma,” amesema Ridhiwani.
Kwa upande wake, Meneja Masoko wa TANESCO, Bw. Fredrick Kalinga, amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kupata elimu kuhusu huduma za shirika hilo ikiwemo miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na maboresho ya mifumo ya kidijitali ya huduma kwa wateja.
Amesema TANESCO pia inaendelea kuhamasisha matumizi ya umeme katika shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia na kwenye vyombo vya usafiri kama magari, bajaji, pikipiki na maguta ya umeme.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2026 yenye kaulimbiu “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu” yalianza Juni 16 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2026.
