Na Mwandishi Wetu, Arusha
Wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kunufaika na fursa za ajira kupitia vikundi vya kijamii vitakavyoshiriki kazi za matengenezo ya kawaida ya barabara chini ya Mradi wa RISE unaotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Mpango huo unahusisha kuunda vikundi vyenye wanachama kati ya watano hadi 20 vitakavyopewa mikataba ya kufanya kazi za kusafisha mitaro, kuziba mashimo madogo, kuondoa vikwazo barabarani, kufyeka majani pamoja na kazi nyingine zisizohitaji matumizi ya mitambo mikubwa.
Mtaalamu wa masuala ya kijamii kutoka TARURA Makao Makuu, Bi. Mwanamisi Abdallah, amesema mpango huo unatekelezwa kwa kuzingatia utaratibu wa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya kazi za barabara kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, huku wananchi wakipewa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika miradi hiyo.
“Vikundi hivi vitasaidia kuongeza ajira, kipato cha wananchi na wakati huohuo kuhakikisha barabara zinabaki katika hali nzuri kwa matumizi ya mwaka mzima,” amesema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Programu kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. Dampu Ndenzako, amesema ushirikiano wa ILO na TARURA unalenga kuhakikisha mfumo huo unawanufaisha wananchi huku ukiimarisha usafiri na usafirishaji hasa maeneo ya vijijini.
Amesema ushiriki wa jamii katika utunzaji wa barabara huongeza umiliki wa miundombinu hiyo na kuhakikisha huduma zinaendelea kupatikana hata katika misimu yenye changamoto za hali ya hewa.
Tayari Wilaya ya Kongwa imeanza kutekeleza mpango huo ambapo vikundi 34 vya CBRM vimeundwa, huku vikundi 31 vikiwa vimeanza kazi na vingine vikikamilisha taratibu za kuingia mikataba.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kongwa, Mhandisi Peter Johnson, amesema hatua hiyo imeanza kuleta fursa za kiuchumi kwa wananchi pamoja na kuimarisha matengenezo endelevu ya barabara.
Mafunzo ya siku sita yanayoendelea Arusha yanawakutanisha wahandisi, wataalamu wa mazingira na jamii wa TARURA pamoja na maafisa maendeleo ya jamii kutoka halmashauri mbalimbali kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa mpango huo katika mwaka wa fedha 2026/27.

