PBPA kutumia Sabasaba kutoa elimu ya mafuta na nishati kwa wananchi


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoshiriki katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF-Sabasaba 2026), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere kuanzia Juni 28 hadi Julai 13. 

Maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha taasisi za umma, sekta binafsi na wananchi kwa ajili ya kuonesha huduma, bidhaa na fursa mbalimbali za maendeleo.

Katika maonesho hayo, PBPA inatumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya kuratibu uagizaji wa mafuta nchini kupitia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS), ambao umeanzishwa ili kuhakikisha Tanzania inapata mafuta ya kutosha, yenye ubora na kwa bei shindani.

Maafisa wa PBPA wanasema wananchi wanaotembelea banda la taasisi hiyo wanapata fursa ya kujifunza namna mfumo huo unavyofanya kazi, mchango wake katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini na hatua zinazochukuliwa kuimarisha usalama wa nishati na uchumi wa taifa.

Mbali na kutoa elimu, PBPA pia inaonesha mafanikio ya taasisi hiyo katika kusimamia uagizaji wa bidhaa za mafuta ikiwemo petroli, dizeli, mafuta ya ndege, gesi ya kupikia (LPG) na bidhaa nyingine za petroli zinazotumika katika shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.


Ushiriki wa PBPA katika Sabasaba 2026 unalenga pia kuimarisha uelewa wa umma kuhusu nafasi ya taasisi hiyo katika kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mafuta, kuchochea maendeleo ya sekta ya nishati na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Wananchi wametakiwa kutembelea banda la PBPA katika maonesho hayo ili kupata elimu, kuuliza maswali na kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania