Na Mwandishi Wetu, Mtwara
Wakazi wa Kata ya Nanhyanga wilayani Tandahimba wameanza kunufaika na huduma bora za usafiri na usafirishaji baada ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kukamilisha ujenzi wa kalavati na matengenezo ya barabara ya Mwindi-Mnauke yenye urefu wa kilomita nane.
Mradi huo uliotekelezwa kupitia Mradi wa RISE chini ya programu ya kuondoa vikwazo vya barabara (Bottleneck) umeondoa changamoto ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa vijiji vya Miule, Nanhyanga na Milongodi, ambavyo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa zao la korosho wilayani humo.
Wakizungumza na maafisa wa Kitengo cha Habari cha TARURA, wananchi wa eneo hilo wamesema miundombinu hiyo imebadili maisha yao kwa kurahisisha usafiri, biashara na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Mkazi wa Kijiji cha Mnauke, Bi. Salma Mwaya, amesema kabla ya mradi huo hali ya barabara ilikuwa mbaya kiasi kwamba hata kuvuka kwa miguu au baiskeli ilikuwa changamoto kubwa.
"Maji yakijaa tulikuwa tunapata shida sana. Watu wa Mwindi waliokuwa wanaenda Nanhyanga kupata huduma za kila siku waliteseka sana," amesema.
Naye Bw. Mustapha Ismail Chilumba amesema kabla ya ujenzi wa daraja na matengenezo ya barabara, wananchi walilazimika kulipa kati ya Sh2,000 na Sh5,000 ili kuvushwa pamoja na mizigo yao.
Amesema wakulima wa korosho walikuwa wakizunguka umbali mrefu kupitia vijiji vya Malamba na Miule ili kufikisha mazao yao maghalani, jambo lililoongeza gharama na muda wa usafirishaji.
"Sasa tunamshukuru sana Rais Samia na Serikali kwa kutatua changamoto hii. Maisha yamekuwa rahisi na usafirishaji wa mazao umeimarika," amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Tandahimba, Mhandisi Innocent Ambrosi, amesema eneo hilo halikupitika wakati wa masika na hata baadhi ya vipindi vya kiangazi kutokana na ubovu wa miundombinu.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kumeleta unafuu mkubwa kwa wananchi wa vijiji vya Mnauke na Mwindi, hususan wakulima wa korosho ambao sasa wanafikisha mazao yao sokoni kwa urahisi zaidi.
"Hii ni barabara muhimu kwa uchumi wa wilaya yetu kwa sababu eneo hili ni mzalishaji mkubwa wa korosho. Mradi huu umefungua mawasiliano na kuchochea shughuli za kiuchumi," amesema.
Mradi wa RISE unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuondoa vikwazo vya usafiri, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii za vijijini.