Serikali imeendelea kupanua fursa za ajira kwa vijana kupitia Programu ya Taifa ya ukuzaji ujuzi, huku vijana 5,746 nchini wakinufaika na mafunzo ya uanagenzi yanayowapa ujuzi wa kazi na uwezo wa kujiajiri.
Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Dkt. Evaline Wilbard Munisi, amesema programu hiyo inalenga kuandaa kizazi cha vijana wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Sengerema mkoani Mwanza, Dkt. Munisi amesema Serikali imeweka mkazo katika ukuzaji wa ujuzi ili kuendana na mahitaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Tunataka kuwa na nguvu kazi yenye maarifa na ujuzi wa kutosha ili kuchochea maendeleo ya taifa na kuongeza ushindani katika soko la ajira," amesema.
Programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, ambapo washiriki hupata mafunzo darasani na mafunzo ya vitendo sehemu za kazi.
Mbali na Serikali kugharamia ada zote za mafunzo, awamu ya sasa ya programu imeongeza huduma ya bima ya afya pamoja na posho ya usafiri ya TShs. 100,000/= kwa mwezi kwa kipindi cha mafunzo ya vitendo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Alana Nchimbi, tangu kuanzishwa kwa programu hiyo mwaka 2016, jumla ya Watanzania 168,657 wamenufaika kupitia mafunzo ya uanagenzi, uzoefu kazini, utambuzi wa ujuzi na uboreshaji wa stadi za kazi.
Katika mwaka wa fedha 2025/26, mafunzo hayo yanatolewa kupitia taasisi 46 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Mkoani Mwanza pekee, vijana 339 wanapitia mafunzo hayo katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Sengerema, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malya na Pine College.
Baadhi ya wanufaika wamesema tayari wameanza kujipatia kipato kupitia ujuzi walioupata, huku wakiiomba Serikali kuongeza ushirikiano na waajiri ili kupanua fursa za mafunzo ya vitendo.
Programu hiyo inaendelea kuonekana kama moja ya silaha muhimu ya Serikali katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuwaandaa kwa uchumi wa kisasa unaohitaji ujuzi zaidi kuliko vyeti pekee.