Daraja la Mkululu lafuta adha ya usafiri, lachochea biashara Masasi

Na Mwandishi wetu

Masasi, Mtwara – Wananchi wa Kata ya Mkululu na maeneo jirani wilayani Masasi wameanza kunufaika na huduma bora za usafiri na usafirishaji baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja kwenye barabara ya Chingutwa–Songambele.

Daraja hilo lililojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia Mradi wa RISE chini ya programu ya kuondoa vikwazo vya barabara (Bottleneck) limeondoa changamoto iliyodumu kwa miaka mingi, hasa katika usafirishaji wa mazao ya kilimo.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Masasi, Mhandisi John Kimario, amesema kabla ya ujenzi huo wakulima walipata ugumu mkubwa wa kusafirisha mazao yao kwenda kwenye maghala na masoko.

"Wilaya yetu inategemea sana kilimo cha korosho, ufuta na mbaazi. Zamani, mvua ziliponyesha magari yalishindwa kupita na mazao yalichelewa kufika maghalani. Sasa hali imebadilika kabisa," amesema.

Ameongeza kuwa daraja hilo limekuwa kiunganishi muhimu kati ya kata za Mkululu, Chingutwa na Lulindi, huku likirahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Wanafunzi pia ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huo.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mkululu, Khalid Masinde, amesema zamani walikuwa wakichelewa kufika shuleni wakati wa masika kwa kusubiri maji yapungue ili wavuke.

"Kwa sasa tunapita bila shida hata mvua zikinyesha. Hatuchelewi tena kufika shuleni," amesema.

Naye mwanafunzi mwenzake, Latifa Rajabu, amesema daraja hilo limewapa uhakika wa kwenda shule kipindi chote cha mwaka.

Kwa upande wa wakazi, Habibu Abdallah, ambaye ni dereva wa bodaboda, amesema biashara yake imeimarika baada ya ujenzi wa daraja hilo.

"Kabla ya daraja, tulikuwa tunasubiri saa nyingi au hata siku mbili mvua zikizidi. Sasa tunafanya kazi bila vikwazo na abiria wanafika wanakokwenda kwa urahisi," amesema.

Wananchi wa Mkululu wanaamini kuwa miundombinu hiyo mpya si tu imeondoa kero ya usafiri, bali pia imefungua fursa mpya za biashara, elimu na maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.