Na Mwandishi wetu
Serengeti Boys wamekosa kombe la Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 baada ya kufungwa kwa penalti 4-2 na Senegal kwenye fainali ya AFCON U17 iliyochezwa Rabat, Morocco.
Tanzania ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la mapema dakika ya saba kupitia Hamis Chenga, kabla ya Senegal kusawazisha dakika ya 64 kupitia Ibrahima Dione.
Baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, mchezo uliamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Senegal walikuwa makini zaidi na kutwaa ubingwa wao wa pili wa mashindano hayo.
Licha ya kukosa kombe, Serengeti Boys wameondoka Morocco wakiwa moja ya timu zilizong'ara zaidi kwenye michuano hiyo.
Kiungo Issa Chole alitangazwa Mchezaji Bora wa Mashindano, huku Dismas Athanasi Elieneza akitwaa tuzo ya Mfungaji Bora.
Madogo wameiheshimisha vyema nchi kwa kushinda tuzo ya Fair Play kutokana na nidhamu nzuri waliyoinyesha uwanjani.
Mafanikio hayo yanaifanya Tanzania kuondoka na tuzo tatu kubwa za mashindano, jambo linaloonyesha ukuaji wa soka la vijana nchini.
Kufika fainali pia kumewapa Serengeti Boys tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la FIFA U17 litakalofanyika Qatar mwaka huuhuu wa 2026.
Ingawa kombe limekwenda Senegal, Tanzania imeondoka na uthibitisho kwamba kizazi kipya cha soka kinaweza kushindana na timu bora kabisa Afrika.
