Bashiru: Wafugaji waheshimu sayansi kuongeza tija

Na Mwandishi wetu 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally amepongeza kiwango cha uwekezaji kilichofanywa katika sekta ya maziwa mkoani Iringa, akisema kinaonesha namna ufugaji wa kisasa na wa kibiashara unavyoweza kuongeza uzalishaji na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Dkt. Bashiru alitoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kukagua shughuli za ufugaji na uzalishaji wa maziwa katika kampuni ya ASAS, akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo.

Alisema mafanikio ya sekta ya mifugo yanategemea matumizi ya sayansi, teknolojia na ushauri wa wataalamu, huku akiwataka wafugaji kuwapa nafasi wataalamu kutumia ujuzi wao ili kuongeza tija.

“Tumeona wataalamu wenye uwezo mkubwa ambao wameajiriwa hapa. Nchi imewekeza katika kuwafundisha wataalamu hawa, hivyo ni muhimu kuwapa nafasi na nyenzo za kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,” alisema.

Waziri huyo pia aliipongeza ASAS kwa uwekezaji katika miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua pamoja na uzalishaji wa malisho ya mifugo, akisema hatua hiyo inaendana na juhudi za Serikali za kuhakikisha wafugaji wanakuwa na uhakika wa chakula na maji kwa mifugo yao mwaka mzima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Deodatus Mwanyika, alisema uwekezaji huo umeipa kamati uzoefu wa vitendo unaoweza kusaidia kutoa ushauri bora kwa Serikali kuhusu maendeleo ya sekta ya maziwa.

“Huu ni uwekezaji ambao Watanzania tunahitaji kuuona. Tuna ardhi ya kutosha, lakini hatujaitumia kikamilifu. Kama tungekuwa na kampuni hata 10 zinazofanya kazi kwa kiwango hiki, sekta ya maziwa ingekuwa imepiga hatua kubwa zaidi,” alisema.

Mkurugenzi wa ASAS, Fuad Jaffer, aliishukuru Serikali kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa kwa wawekezaji katika sekta hiyo. Alisema pamoja na uzalishaji wa maziwa, kampuni hiyo imejipanga kuongeza uzalishaji wa mitamba bora ili kuwasaidia wafugaji kupata mbegu bora za ng’ombe wa maziwa.

Ziara hiyo pia ilihusisha kutembelea shamba la mifugo na kiwanda cha kusindika maziwa cha Shafa pamoja na shamba la mfugaji Richard Philips maarufu kama Kibebe.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kibebe aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng’ombe, hatua ambayo amesema imechangia kulinda mifugo na kuongeza uzalishaji.

Ziara ya viongozi hao ni sehemu ya maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Maziwa yanayofanyika katika Viwanja vya Mwembetogwa mkoani Iringa, huku kilele chake kikitarajiwa kufanyika Juni 1, 2026.