SERIKALI NA BMT WAIDHINISHA HAJI MANARA KUWA MSEMAJI WA TIMU ZA TAIFA


Na Mwandishi Wetu 

Serikali imemteua Haji Manara kuwa msemaji rasmi wa timu za taifa za mpira wa miguu nchini Tanzania.

Uteuzi huo ulitangazwa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda jijini Dodoma. 

Kwa mujibu wa serikali, Haji Manara atafanya kazi chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na atasimamia mawasiliano ya timu zote za taifa za soka. 

Akizungumza na waandishi wa habari, leo, jijini Dar es salaam baada ya uteuzi huo, Manara alimshukuru Mungu pamoja na serikali kwa kumuamini kwenye nafasi hiyo mpya.

“Alhamdulillah kwa leo kuwa hapa. Lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia mimi kuteuliwa na serikali yangu,” alisema.

Hii inahesabika kama 'comeback' nyingine kubwa kwa Manara ndani ya mpira wa miguu nchini.


Kwa miaka kadhaa, Manara amekuwa mmoja wa watu maarufu zaidi kwenye vyombo vya habari vya soka nchini baada ya kufanya kazi ya uhamasishaji akiwa na vilabu vya Simba SC na baadaye Yanga SC.

Style yake ya kuhamasisha, kupiga promo na kuleta hamsha hamsha ya aina yake, tena kubwa na ya kipekee kwa mashabiki ilifanya jina lake kuwa moja ya majina makubwa kwenye mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.

Uteuzi wake unakuja wakati Tanzania ikiendelea kujiandaa na AFCON 2027 ambayo itaandaliwa kwa pamoja na nchi za Kenya na Uganda. 

Taifa Stars pia ipo kwenye kipindi cha kujijenga chini ya kocha wake Miguel Gamondi ambaye aliteuliwa rasmi Februari mwaka huu baada ya kuiongoza Tanzania kufika hatua ya 16 bora AFCON 2025 kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi.