Na Mwandishi wetu, kongwa
Wananchi na wawekezaji katika wilaya za Kongwa, Chamwino, Mpwapwa, Kiteto na Gairo wanatarajiwa kunufaika na huduma bora zaidi ya umeme baada ya TANESCO kukamilisha miradi ya kuboresha miundombinu ya umeme yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 10.5.
Miradi hiyo iliyozinduliwa Juni 16, 2026 na Waziri wa Nishati, Dkt. Deogratius Ndejembi katika eneo la Mbande wilayani Kongwa, inajumuisha ujenzi wa kituo cha kubadilishia njia za usambazaji wa umeme, transfoma ya kisasa ya kudhibiti msongo wa umeme yenye uwezo wa MVA 20 pamoja na njia ya umeme ya kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 92 kutoka Zuzu hadi Mbande.
Waziri Ndejembi amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika unaochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema hapo awali hitilafu katika eneo moja ilikuwa ikisababisha kukatika kwa umeme katika maeneo mengine, hususan wakati wa mvua, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za wananchi na biashara.
“Leo tunashuhudia matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya nishati inayokwenda kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesema Ndejembi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Lazaro Twange amesema kwa miaka mingi wilaya hizo zilitegemea njia moja ya umeme ya kilovoti 33 kutoka Dodoma, jambo lililosababisha changamoto kadri mahitaji ya umeme yalivyoongezeka.
Amesema tangu miradi hiyo ianze kufanya kazi, kukatika kwa umeme katika maeneo hayo kumepungua kwa zaidi ya asilimia 90, hatua inayotoa uhakika mkubwa kwa wananchi na wawekezaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amesema maboresho hayo yanaonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kutatua changamoto za umeme na kuboresha huduma kwa wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka, amewataka wananchi kutumia fursa ya umeme wa uhakika kuanzisha viwanda vidogo, shughuli za uchakataji wa mazao na biashara nyingine zitakazoongeza kipato na ajira.
Miradi hiyo inatarajiwa kuongeza kasi ya uwekezaji, kukuza shughuli za viwanda, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuimarisha uchumi wa maeneo ya Kanda ya Kati.


