TASUBA kuwaandaa vijana kufahamu biashara ya muziki na filamu

Na Mwandishi wetu

Bagamoyo. Wanafunzi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) wanatarajiwa kupata maarifa kuhusu biashara ya muziki, filamu na uchumi wa ubunifu kupitia mjadala maalum wa Music & Film Business Session utakaofanyika Juni 19, 2026 katika ukumbi wa taasisi hiyo.

Mjadala huo unalenga kuwajengea wanafunzi na wabunifu vijana uelewa kuhusu namna ya kuendesha taaluma za ubunifu kwa mtazamo wa kibiashara, ikiwemo kujenga mitandao ya kitaaluma, kutambua fursa za kazi na biashara pamoja na kujifunza namna ya kuendeleza vipaji vyao kwa muda mrefu.

Miongoni mwa wazungumzaji watakaoshiriki ni mtaalamu wa biashara ya muziki na meneja wa msanii Alikiba, Benjamin Otwal, pamoja na wadau wa sekta ya filamu akiwemo Rais Mstaafu wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Eliya Mjatta, na mtangazaji wa televisheni na muigizaji, Conrad Kashasha.

Mratibu wa tukio hilo, Stellabeatrice Benedict, ambaye pia ni mhitimu wa TASUBA katika fani ya Uzalishaji wa Filamu na Televisheni, amesema lengo ni kuwasaidia vijana kutambua kuwa mafanikio katika tasnia za ubunifu hayategemei kipaji pekee bali yanahitaji pia maarifa ya biashara, ujenzi wa mahusiano ya kitaaluma na uwezo wa kutumia fursa zilizopo.

“Vijana wengi wenye vipaji wanahitaji pia maarifa ya biashara na mbinu za kujenga taaluma imara kwa muda mrefu. Kupitia mjadala huu tunatarajia kuwapa mwanga na kuwaunganisha na wataalamu waliopo kwenye tasnia,” amesema Stellabeatrice.

Amesema Music & Film Business Session ni sehemu ya juhudi za kuendeleza mazungumzo kuhusu uchumi wa ubunifu na kuwawezesha vijana kujenga ajira na biashara endelevu katika sekta za muziki, filamu na sanaa kwa ujumla.