TARURA na JKCI waimarisha afya za watumishi kwa elimu na uchunguzi wa mara kwa mara

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wameendesha semina maalum ya afya kwa watumishi wake, ikilenga kuongeza uelewa kuhusu magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza pamoja na umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

Semina hiyo iliyofanyika katika Makao Makuu ya TARURA jijini Dodoma, ilijikita katika magonjwa kama shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kisukari, homa ya ini pamoja na mbinu za kujikinga dhidi ya changamoto mbalimbali za kiafya.

Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TARURA, Bi. Azimina Mbilinyi, amesema taasisi hiyo inaendelea kuweka ustawi wa watumishi kuwa kipaumbele kwa kutambua kuwa afya bora ndiyo msingi wa utendaji kazi wenye tija.

“TARURA imeendelea kuandaa programu mbalimbali za afya ikiwemo semina na upimaji wa afya kila robo ya mwaka ili watumishi wajue hali zao za kiafya na kujikinga na magonjwa mbalimbali,” amesema.

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya taasisi ya kuboresha ustawi wa watumishi waliopo Makao Makuu na katika ofisi za mikoa kote nchini.

Mbali na kupata elimu, watumishi walipata nafasi ya kupima viashiria muhimu vya afya ikiwemo presha, kiwango cha sukari mwilini, afya ya moyo, uzito na urefu, sambamba na kupatiwa ushauri wa kitaalamu kulingana na matokeo yao.

Kwa upande wake, Daktari Janet Mmari kutoka JKCI amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kubaini mapema changamoto za kiafya kabla hazijawa kubwa.

Amewahimiza watumishi kufanya mazoezi, kula lishe bora na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kupunguza hatari ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Watumishi wa TARURA waliohudhuria semina hiyo wameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kubadili mtindo wa maisha, kutunza afya zao na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.