Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imezindua mpango maalumu wa miaka mitatu wa kuokoa aina 57 za miti ya asili iliyo katika hatari kubwa ya kutoweka, katika juhudi za kulinda bioanuwai ya Tanzania dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa misitu na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali.
Hatua hiyo inakuja wakati zaidi ya aina 376 za miti nchini zimeorodheshwa katika Orodha Nyekundu ya Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) zikiwa katika viwango mbalimbali vya hatari ya kutoweka.
Akizindua mradi wa Enhanced Conservation of 57 Highly Threatened Tanzanian Tree Species jijini Dodoma, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, John Elia, amesema uhifadhi wa spishi hizo ni muhimu kwa kulinda urithi wa mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Tanzania imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa bioanuwai, lakini baadhi ya miti yetu adimu inakabiliwa na vitisho mbalimbali. Mradi huu ni hatua muhimu kuhakikisha spishi hizi zinaendelea kuwepo kwa manufaa ya taifa,” amesema.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), huku ukifadhiliwa na Franklinia Foundation pamoja na Missouri Botanical Garden kwa zaidi ya dola za Marekani 390,000.
Mratibu wa mradi huo, ambaye pia ni Kamishna Msaidizi Muandamizi na Meneja wa Biolojia ya Mbegu za Miti TFS, Fandey Mashimba, amesema shughuli zitakazofanyika ni pamoja na ukusanyaji wa mbegu, uzalishaji wa miche, utafiti wa kisayansi, kurejesha makazi ya asili ya miti hiyo na kuimarisha uwezo wa wataalamu wa uhifadhi.
Amesema mradi huo hauishii kuokoa miti 57 pekee, bali utaweka msingi wa mbinu bora za kuokoa spishi nyingine za miti zinazokabiliwa na hatari ya kutoweka nchini.
Uzinduzi huo umehusisha wataalamu wa misitu, watafiti pamoja na wadau wa uhifadhi kutoka Tanzania na nje ya nchi, wakisisitiza umuhimu wa kulinda misitu kama ngao muhimu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa viumbe hai.

