Na Mwandishi Wetu, Arusha
Wataalamu wa maabara nchini wametakiwa kuongeza umakini katika uhifadhi wa vimelea hatarishi na sampuli za muda mrefu ili kuzuia hatari zinazoweza kuhatarisha afya ya jamii.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Afya kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bi. Valentino Sanga, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku tano kinachowakutanisha wataalamu wa maabara jijini Arusha.
Bi. Sanga amesema wataalamu hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha mifumo ya usalama wa maabara inaimarishwa, ikiwemo utambuzi wa mapema wa vihatarishi na utunzaji salama wa vimelea vinavyoweza kusababisha milipuko ya magonjwa.
“Tunapaswa kuzingatia maadili na viapo vya taaluma zetu kwa sababu uzembe katika utunzaji wa vimelea unaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi,” amesema.
Mafunzo hayo yanatoa fursa kwa wataalamu kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mpya zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa katika usimamizi wa usalama wa maabara.
Kwa upande wake, mwakilishi wa taasisi ya Center for International Health, Education and Biosecurity Tanzania (CIHEB-Tanzania), Bw. Samwel Mulungu, amesema usalama wa vimelea vinavyohifadhiwa maabara ni suala nyeti linalohitaji uangalizi wa hali ya juu.
Amesema historia imeonyesha kuwa hitilafu katika mifumo ya usalama wa maabara inaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya, ikiwemo kuenea kwa maambukizi ya vimelea hatari kama kimeta.
“Usalama wa maabara si jukumu la wataalamu pekee, bali ni sehemu muhimu ya kulinda afya ya taifa,” amesema.
Mafunzo hayo yanaungwa mkono kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security – GHS) na yamewakutanisha wataalamu 26 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya, Maabara ya Taifa, hospitali za mikoa na rufaa, pamoja na taasisi mbalimbali zinazohifadhi vimelea na sampuli za muda mrefu.

