TFRA yasogeza huduma za mbolea karibu na wananchi Wiki ya Utumishi wa Umma Dodoma


Na Mwandishi wetu

Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imewataka wakulima, wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya mbolea kutembelea banda lake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Kupitia maonesho hayo yanayofanyika kuanzia Juni 16 hadi 23, 2026, TFRA itatoa huduma mbalimbali ikiwemo utoaji wa vibali vya kuingiza na kusafirisha mbolea nje ya nchi, usajili wa biashara za mbolea pamoja na elimu kuhusu matumizi sahihi na uhifadhi wa mbolea.

Wananchi watapata pia taarifa kuhusu mafunzo ya biashara ya mbolea, huduma za uchunguzi wa ubora wa mbolea maabara pamoja na fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea na viwanda vinavyounga mkono sekta hiyo.

Aidha, wakulima wataweza kupata huduma ya usajili na uhuishaji wa taarifa zao katika mfumo wa ruzuku ya pembejeo za kilimo ili kuendelea kunufaika na programu za Serikali za kuwasaidia kuongeza uzalishaji.

TFRA imesema ushiriki wake katika maonesho hayo unalenga kuwasogezea wananchi huduma za udhibiti na maendeleo ya sekta ya mbolea kwa karibu, sambamba na kutoa majibu ya maswali mbalimbali yanayohusu biashara na matumizi ya mbolea nchini.

“Usibaki na maswali kuhusu sekta ya mbolea. Tembelea banda la TFRA Chinangali Park, Dodoma, upate huduma na elimu sahihi kutoka kwa wataalamu wetu,” imesema mamlaka hiyo.

Maonesho ya mwaka huu ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanafanyika chini ya kaulimbiu inayohamasisha uwajibikaji shirikishi kwa utoaji wa huduma bora na endelevu kwa wananchi.

TFRA inaendelea kuhimiza matumizi ya mbolea zenye ubora kwa lengo la kuongeza tija katika kilimo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia kaulimbiu yake ya “Mbolea Bora kwa Kila Mkulima.”