Na Mwandishi wetu
Nyasi zishaanza kutikiswa nchini Marekani, Canada na Mexico, lakini katika ulimwengu wa data na akili mnemba (AI), Kombe la Dunia la 2026 tayari limeshapata bingwa.
Mifumo mbalimbali ya uchambuzi wa takwimu na kompyuta imeendesha majaribio ya mamilioni ya matukio ya mechi (simulations) ili kutabiri nani ana nafasi kubwa ya kubeba kombe, na ni Hispania.
Mfumo maarufu wa Opta Supercomputer, ambao uliendesha takribani simulations 25,000, uliipa Hispania nafasi kubwa zaidi ya kutwaa taji kwa asilimia 16.1.
Timu hiyo inafuatwa kwa karibu na mataifa yenye nguvu ya soka duniani kama Ufaransa, Uingereza na mabingwa watetezi Argentina.
Ukiachana na hao, manguli wa michezo ya video (videogames) EA Sports pia iliendesha Kombe la Dunia la 2026 ndani ya mfumo wake wa mchezo, ikichezesha mechi zote 104 za mashindano hayo. Matokeo yake nayo yalimuona Hispania akiibuka bingwa.
Utabiri wa EA Sports unaaminika na wengi kutokana na historia yao (EA Sports) ilivyofanikiwa kutabiri mabingwa wa Kombe la Dunia wa mwaka 2010, 2014, 2018 na 2022 kupitia mifumo yake ya simulation.
Aidha, mifumo mingine inayotumia mbinu za Monte Carlo AI, ambayo huendesha maelfu ya matukio tofauti kwa kuzingatia viwango vya timu, uwezo wa wachezaji, historia ya matokeo na mambo mengine ya takwimu, pia imeonyesha Hispania akiwa mbele kwa nafasi sawa ya karibu asilimia 16.1 ya kushinda.
Hata hivyo, tunawakumbusha kuwa simulation si unabii.
Kwa mfano, uwepo wa asilimia 16.1 inamaanisha kuwa hata timu inayotajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi bado ina uwezekano mkubwa wa kutoshinda kuliko kushinda.
Vitu kama vile majeruhi, viwango vya wachezaji, maamuzi ya makocha na marefa uwanjani yanaweza kubadilisha kila kitu ndani ya dakika 90.
Data zinamuaminisha Hispania. Lakini mpira huamuliwa uwanjani.


