Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakati Tanzania ikiendelea kupanua fursa za elimu na ulinzi wa watoto, takwimu zinaonesha kuwa changamoto ya utumikishwaji wa watoto bado ipo, huku asilimia 25.8 ya watoto nchini wakihusika katika ajira za utotoni kwa mujibu wa Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi wa mwaka 2024.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa vita dhidi ya tatizo hilo bado ina safari, licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto yaliyofanyika Juni 12, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Dkt. Deus Sangu amesema Serikali imeweka mkakati wa kupunguza kiwango hicho hadi kufikia sifuri ifikapo mwaka 2030 kupitia Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Mtoto wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30.
Sangu amesema utumikishwaji wa watoto si suala la ajira pekee, bali ni changamoto inayonyima watoto haki ya kupata elimu, malezi bora na nafasi ya kuendeleza vipaji vyao.
“Mtoto anapokosa nafasi ya kusoma na kuendeleza uwezo wake, taifa linapoteza rasilimali muhimu ya baadaye,” amesema.
Kwa mujibu wa takwimu za awali zilizowahi kutolewa nchini, takribani watoto milioni 4.2 wenye umri wa miaka 5 hadi 17 walikuwa wakijihusisha na ajira za utotoni mwaka 2014, hali inayoonesha ukubwa wa changamoto ambayo Tanzania imekuwa ikikabiliana nayo kwa miaka mingi.
Sekta zinazotajwa kuwa na hatari kubwa ya utumikishwaji wa watoto ni pamoja na kilimo, uvuvi, migodi, kazi za majumbani pamoja na shughuli mbalimbali za biashara zisizo rasmi.
Sangu amesema tatizo hilo pia lina athari kwa uchumi wa taifa kwani bidhaa zinazozalishwa kwa kukiuka haki za watoto zinaweza kukosa ushindani katika baadhi ya masoko ya kimataifa yenye viwango vya juu vya haki za binadamu.
Katika kuimarisha mapambano hayo, Serikali imeendelea kushirikiana na waajiri, vyama vya wafanyakazi, Shirika la Kazi Duniani (ILO) na wadau wengine kuweka mifumo ya kuzuia watoto kuingia kwenye kazi hatarishi.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu inayosema “Red Card to Child Labour: Fair Play for Children, Decent Work for Adults,” ikisisitiza umuhimu wa watoto kupata haki ya kukua, kusoma na kutimiza ndoto zao huku watu wazima wakipata kazi zenye staha.
