Na Charles Mkoka
Dar es Salaam – Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Tanzania (SiTE) yanatarajiwa kurejea mwaka huu yakiwa na lengo la kuvutia wanunuzi wakubwa na wawekezaji kutoka masoko mbalimbali duniani.
Waandaaji wa maonesho hayo, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), wamesema mfumo wa usajili umeboreshwa, ambapo washiriki sasa wanaweza kujisajili, kutuma maombi na kufanya malipo yote kwa njia ya mtandao.
TTB imeeleza kuwa toleo la mwaka huu litawakutanisha waoneshaji wa Tanzania na wanunuzi wenye kampuni kubwa kutoka Ulaya, Marekani na Asia, ili kuongeza fursa za biashara na ushirikiano katika sekta ya utalii.
Kupitia mfumo huo, waoneshaji wataweza kuona wasifu wa kampuni zitakazoshiriki kabla ya maonesho kuanza, jambo litakalowasaidia kupanga mikutano ya kibiashara na kutafuta washirika wanaowafaa.
Hadi mwezi Juni, zaidi ya wanunuzi 50 wa kimataifa walikuwa tayari wamethibitisha kushiriki, wakiwemo kutoka Urusi, India, China na Korea Kusini.
Waandaaji wanasema SiTE 2026 itakuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika, huku maandalizi yakiendelea kuelekea AFCON 2027, ambayo inatarajiwa kuongeza idadi ya wageni na wawekezaji nchini.
Wadau wa sekta ya utalii wamehimizwa kujisajili mapema kupitia tovuti rasmi ya TTB, huku waandaaji wakieleza kuwa maombi yanaendelea kuwasili kwa kasi na matarajio ni kuwa maonesho ya mwaka huu yatakuwa miongoni mwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini.
