Na Mwandishi wetu
Kampuni ya huduma za malazi na utalii ya Wellworth Collection imetumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuhamasisha utalii wa ndani huku ikiendelea kupanua uwekezaji wake kuelekea fursa za AFCON 2027.
Akizungumza katika banda la Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ofisa Mauzo wa kampuni hiyo, Sharmila Omari, amesema Wellworth Collection inawaalika Watanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kupitia hoteli, lodge na kambi zake zilizopo nchini.
Amesema kampuni hiyo kwa sasa inasimamia lodge tano za nyota tano, kambi nne za kifahari na resort mbili, ikiwemo moja iliyopo Zanzibar, huku resort nyingine ikikamilishwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wake, kampuni hiyo pia inaendelea kuitangaza Mikumi, akibainisha kuwa usafiri umeimarika kufuatia upanuzi wa huduma za SGR, jambo linalorahisisha safari kwa watalii wa ndani.
Katika maonesho hayo, Wellworth Collection inatoa ofa maalum za malazi kuanzia Sh762,000 kwa watu wawili, zikiwa zinajumuisha huduma za chakula.
Sharmila amesema kampuni hiyo pia inamiliki Kunduchi Wet 'N' Wild na imeendelea kuandaa vifurushi vinavyounganisha utalii wa hifadhi za wanyamapori na fukwe za bahari.
Ameongeza kuwa Wellworth Collection inaendelea kujenga lodge na kambi mpya katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ili kuongeza uwezo wa kupokea wageni wanaotarajiwa kuwasili wakati wa mashindano ya AFCON 2027.
"Tunajiandaa kupokea wageni wengi zaidi kuelekea AFCON 2027. Tunawahimiza Watanzania na wageni kufanya nafasi mapema ili kunufaika na ofa zilizopo," amesema Sharmila
