Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi kuhakikisha wanakopa kupitia taasisi za fedha zilizosajiliwa na kusimamiwa na benki hiyo, ikionya kuwa wakopeshaji wasio na leseni wanaweza kuwaweka wananchi katika hatari za kifedha na kisheria.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha BoT, Mwile Kauzeni, amesema benki hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma salama za kifedha na umuhimu wa kukopa kwa malengo.
Amesema BoT inapokea malalamiko kutoka kwa wananchi waliokopa kwa taasisi ambazo hazijasajiliwa, hali inayowanyima ulinzi wa kisheria na kuwafanya kuwa katika mazingira hatarishi.
"Kabla ya kukopa, hakikisha taasisi unayokwenda imeidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania. Orodha ya taasisi zote zilizosajiliwa inapatikana kwenye tovuti ya BoT," amesema Kauzeni.
BoT pia imeonya watu wanaoendesha shughuli za mikopo midogo bila leseni kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai linaloweza kuadhibiwa kwa faini, kifungo au vyote kwa pamoja.
Wakati huo huo, benki hiyo inaendelea na kampeni ya elimu ya fedha ya "Zinduka, Kopa kwa Malengo", inayowahimiza wananchi kukopa kwa ajili ya shughuli zenye tija kama kukuza biashara, kuongeza mtaji au kuwekeza katika kilimo, badala ya kukopa bila mpango wa marejesho.
Kwa mujibu wa BoT, kampeni hiyo tayari imefanyika Dar es Salaam na Mwanza, huku mkoa wa Mbeya ukiwa hatua inayofuata katika kuendelea kuwajengea wananchi uelewa wa matumizi sahihi ya huduma za kifedha.
