Mahe, Ushelisheli
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 69 wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) Kamisheni ya Afrika uliofanyika mjini Mahe, nchini Ushelisheli.
Mkutano huo ulifunguliwa Julai 2, 2026 na Rais wa Ushelisheli, Dkt. Patrick Herminie, ukiwa na kaulimbiu ya "Kuimarisha Rasilimali Watu ili Kuchochea Ukuaji wa Utalii Barani Afrika."
Viongozi wa sekta ya utalii kutoka nchi mbalimbali za Afrika walijadili hali ya utalii barani humo na duniani, ikiwemo mwenendo wa ukuaji wa watalii, fursa za uwekezaji, changamoto zinazoikabili sekta hiyo na namna ya kukuza utalii endelevu.
Mkutano huo pia ulijadili maendeleo ya rasilimali watu, matumizi ya teknolojia na ubunifu katika sekta ya utalii pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama ili kuongeza mchango wa utalii katika uchumi wa Afrika.
Aidha, nchi wanachama zilijadili umuhimu wa kurahisisha usafiri ndani ya bara la Afrika, ikiwemo kuongeza muunganiko wa safari za ndege na kurahisisha upatikanaji wa visa ili kuchochea ukuaji wa utalii wa ndani ya bara.
Kupitia mkutano huo, Mkurugenzi wa UN Tourism Kanda ya Afrika, Elcia Grandcourt, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Afrika wa mwaka 2025/26, uliolenga kukuza utalii endelevu, kuimarisha uwezo wa rasilimali watu, kuongeza uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Tanzania imeendelea kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa ya utalii huku ikiendelea kutangaza vivutio vyake na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.